Nchi
za Jumuaya ya Afrika Mashariki (EAC)
zimeshauriwa kujenga viwanda vingi ili kukwepa kutengeneza soko kwa ajili ya
nchi zingine zenye nguvu duniani.
Ushauri
huo umetolewa na mfanyabiashara
bilionea wa Tanzania, Ali Mufuruki (pichani) ambaye pia ni Mkurugenzi mwanzilishi wa
Kampuni ya Infotech Investment Group Ltd na kusema kuwa kuna fursa za kutosha kwenye Jumuiya hii..
Bw. Mafuruki
amesema kuwa soko la Afrika Mashariki lina watu zaidi ya milioni 160
likiunganishwa na ushirikiano wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki. Lakini
soko lililosainiwa jijini Kigali katika Mkutano wa Machi 21 ni kubwa mara nane
ya soko la Afrika Mashariki.
Mufuruki
amesema, katika miaka 20 iliyopita kuna ongezeko kubwa la biashara kati ya nchi
zote sita za Afrika Mashariki kutokana na ushirikiano mzuri na unaochagizwa na
kuwa na eneo moja la forodha.
Biashara hiyo
pia imeimarika pia kutokana na kupunguzwa kwa vikwazo vya kibiashara katika
mipaka vilivyokuwa vikikabili nchi hizi na kufanya kuwa rahisi kwa wananchi wa
nchi hizo kufanya biashara au kufanya kazi katika nchi nyingine.
Kulingana na
mkataba uliotiwa saini mjini Kigali, utatengeneza soko kubwa karibu mara nane
ya soko la Afrika Mashariki.
Ni soko kubwa
zaidi la watu zaidi ya bilioni 1.2. Katika soko hilo watu wataweza kuuza bidhaa
kutoka nchi moja kwenda nyingine lakini pia kuhama kutoka nchi moja na nyingine
kutafuta kazi na kuanzisha makazi au makampuni ya kibiashara.
“Kwa hiyo
kupanuka kwa soko katika bara la Afrika kuwa kubwa kiasi hicho kutakuwa na
manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,”
alisema Mufuruki.
Alisema nchi
za EAC zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa viwanda vyao kabla ya kuingia
katika soko huria lililosainiwa mjini Kigali.
Bilionea huyo
amesema nchi za EAC zisipojenga viwanda vingi, kuna hatari ya kuwapanulia soko
watu wengine kutoka mataifa makubwa kwa kuwa soko litakuwa wazi, lakini
watakaonufaika watakuwa ni watu wengine.
“Kuna haja ya
nchi za Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa zinajenga viwanda vya kutosha ili
tukiuziana vitu basi tuwe tunauziana vitu vyetu na sio kuuziana vitu vya
wachina au vya Waingereza, Wajerumani au Wamarekani,” aliongeza Mufuruki.
Aidha,
alisema ni vizuri kuuziana vitu vilivyotengenezwa Afrika Mashariki kutoka nchi
moja kwenda nchi nyingine, hapo ndipo zinaweza kutengeneza faida.
Mufuruki
alisema kinyume na hapo nchi hizo zitakuwa zimewatengenezea watu wengine
mazingira mazuri ya biashara na kuwa hatari kwao wenyewe.
Pia katika
makubaliano hayo nchi za Afrika Mashariki zina nafasi ya kutengeneza ajira
kutokana na kufunguliwa milango ya soko huria katika nchi za Afrika.
Hii pia ni
nafasi kwa kampuni za Afrika Mashariki kuwekeza katika mataifa mengine ya
Afrika kutokana na soko kubwa litakalopatikana kutokana na makubaliano ya
Kigali.
Amezisihi
nchi za Afrika Mashariki kutumia nafasi hiyo ya kuwa na soko huria na kuweka
mawazo chanya mbele kuwa zinaweza kufanya biashara ya ushindani na nchi zingine
kama Nigeria, Afrika Kusini, Misri na nyingine.
No comments:
Post a Comment