Tundu Lissu, Rais wa TLS (Getty Image) |
Akizungumza kutoka Jiji la Brussels, Ubelgiji, leo asubuhi, Lissu alisema mchakato na matokeo ya uchaguzi huu yameonesha namna serikali inavyotumiwa vibaya na chama tawala; Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ameilaumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kusimamia
vyema uchaguzi huo na kudai kuwa imekuwa ikisikiliza na kutenda kulingana na
matakwa ya CCM.
“Huo ulikuwa uchaguzi wa mtutu wa bunduki, siyo uchaguzi huru
na wa haki, inasikitisha sana kuwa tabia ya kuvuruga kila uchaguzi inaota
mizizi Tanzania na huenda ikawa na matokeo mabaya zaidi huko mbele ya safari,”
alisema Lissu.
Lissu ambaye yuko Brussels kwa matibabu zaidi baada ya
kushambuliwa na kuumiza kwa risasi na wanaotajwa kuwa ni “watu wasiojulikana,”
alisema anaamini kuwa uchaguzi ungesimamiwa kwa haki, Chadema, kingeibuka na
ushindi.
“Huo haukuwa uchaguzi. Ilikuwa ni vita kati ya serikali na
vyombo vyake vya usalama, tume ya uchaguzi na muundo wake wote na CCM kwa
upande mmoja; dhidi ya Chadema na wananchi kwa upande mwingine” aliongeza Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).
Lissu alisema kwa kuwa uchaguzi huo uligeuka kuwa vita, ndiyo
maana matokeo yake hayakukubalika na watu wenye dhamana ya kulinda usalama wa
wapigakura na wananchi, walitumia silaha za moto kuwatisha.
“Inashangaza kuwa Tanzania sasa inatumbukia kwenye shimo baya
sana la kuua raia, kisa; siasa na uchaguzi ambao ukiendeshwa vyema na kwa haki,
hakuna matatizo yoyote yanayoweza kutokea,” alisema Lissu.
Lissu anatibiwa Ubelgiji baada ya Septemba 7, mwaka jana
kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa Mjini Dodoma, ambako alikuwa
akihudhuria vikao vya bunge. Alipigwa risasi 38 akiwa nje ya nyumba yake, huku
risasi 8 zikiingia mwilini mwake na kuvunja mifupa na kuharibu nyama za mwili.
Tayari Chadema na vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi wa
majimbo hayo, Kinondoni na Siha, vimelalamikia kutofanyika kwa uchaguzi huru na
haki na kuitupia lawama serikali, hasa Jeshi la Polisi na tume ya uchaguzi.
Chadema, kama ilivyotokea kwa Chama cha Wananchi (CUF),
kimeilalamikia NEC kwa kuwanyima vitambulisho mawakala wao mpaka dakika za
mwisho; kuzuiliwa kuingia vituoni na hata polisi kudaiwa kuwapiga mawakala wao.
Marudio ya uchaguzi wa Kinondoni na Siha ulifanyika juzi -
Februari 17, huku wabunge wa CCM wakiibuka washindi. Pia kata 10 zilifanya
uchaguzi maeneo mbalimbali ya Tanzania
No comments:
Post a Comment