Mitungi ya Gesi |
Taasisi
za Serikalizi zimepIgwa mafuruku kutumia mkaa na badala yake zimepewa muda wa
mwaka mmoja kujiandaa kuhamia kwenye
nishati ya gesi na mkaa mbadala ili kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia
Muungano na Mazingira January Makamba wakati wa upandaji miti kuendeleza
programu ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani lililofanyika katika Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM).
Alisema
miongoni mwa taasisi hizo ni magereza, shule, vyuo na hospitali nchini ambazo
zinatumia mkaa kupikia. January alisema ofisi yake inatarajia kutoa waraka na
kwamba asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa kupikia na kumuagiza Katibu
Mkuu wa wizara hiyo kuandaa mkakati wa kupunguza matumizi ya mkaa nchini.
“Tunazitaka
taasisi za umma ziache kutumia mkaa tutatoa tamko hilo rasmi kwa waraka hata
wazabuni hawatapata zabuni kama hawatatumia gesi. Kifungu cha 13 cha sheria ya
mazingira, waziri mwenye dhamana ya mazingira ana uwezo wa kutoa maelekezo
kufanya jambo litakalookoa mazingira,” alisema January.
“Mkaa ni
nishati yenye gharama kushinda sehemu yoyote, maisha ya watu wa vijijini
yanazidi kuharibiwa kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema. Kwa upande
wake, Naibu Waziri wake, Kangi Lugola alisema serikali haitawavumilia
wawekezaji
katika nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vinavyotiririsha kemikali za sumu kwa
kisingizio cha sera ya Tanzania ya viwanda.
“Serikali
haitawafumbia macho watu wote wanaoharibu mazingira kwa kisingizio cha sera ya
Tanzania ya Viwanda. Watu wamejisahau sana wanajua wanaweza kuishi bila kutunza
mazingira,” alisema Lugola.
Alisema wapo
watu binafsi na kampuni wanawekeza katika sekta mbalimbali, lakini wamekuwa hawazingatii
utunzaji wa mazingira. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira, Joseph Malongo alisema awamu ya pili ya zoezi la upandaji miti
litafanyika kwenye barabara zote zinazoingia mkoani Dodoma.
Naye Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma
Mjini, alisema jimbo lake linatekeleza programu ya upandaji miti kwa kila kata
na kwamba utunzaji mazingira wao kama viongozi wa kisiasa wameifanya kama
ajenda ya kudumu kwenye mikutano yao ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Makamu Mkuu
wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema miti 30,000 itapandwa katika maeneo
ya chuo hicho huku akihimiza wanachuo kutunza mazingira na kwamba wameunda
kikosi kazi cha kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii inayozunguka
chuo.
Kadhalika,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira,
Sadiq Murad alisema sera ya viwanda iende sambamba na utunzaji mazingira kwa
kuwa viwanda vimekuwa havitunzi mazingira huku akitoa angalizo kwa chuo hicho
kuhakikisha miti iliyopandwa inastawi.
Upandaji huo
wa miti ni utekelezaji wa kampeni ya Kijanisha Dodoma iliyozinduliwa na Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan
No comments:
Post a Comment