Lango la Kuingilia kwenye Majengo ya Mlimani City Mall |
Mkataba baina ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mradi wa Mlimani City, Kampuni ya Mlimani City Holdings LTD iliyo chini ya Kampuni ya A Turnstar Holdings Group ya Botswana.Umeikasirisha amati ya Bunge ya Hesabu zaSerikali (PAC) baada ya kubaini 'madudu' kwenye mkataba huo.
Kauli hiyo imetolewa kwenye kikao cha
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo hata hivyo iliagiza
watendaji wa chuo hicho, waliosaini na mwekezaji huyo mwaka 2004 kwenda Dodoma
kwa mahojiano zaidi.
Moja ya Majengo ya UDSM |
Hatua hiyo ilifikiwa ikiwa ni baada ya kikao
cha saa tano, kati ya wajumbe wa kamati hiyo na uongozi wa sasa wa chuo hicho.
Walianza kwa kukagua eneo la miradi na kisha majadiliano. Moja ya upungufu
ambao kamati hiyo ilibaini ni ucheleweshaji wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu
katika eneo la mradi na utengenezwaji wa bustani ya kisasa, itakayokuwa na
wanyama wa aina mbalimbali.
Lakini, kitu kilichowatia hasira zaidi wajumbe
wa kamati hiyo ni mradi huo kutokinufaisha chuo hicho, huku mwekezaji huyo
aliyeingia nchini mwaka 2004 akiwa na mtaji wa Dola za Marekani 75 sawa na Sh
150,000, akilalamika kuwa hapati faida.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka pamoja na wajumbe wake walihamaki baada ya kubainisha udhaifu kwenye
mkataba huo, ambapo Mbunge Catherine Ruge wa Viti Maalumu (Chadema)
alishangazwa kwa Chuo Kikuu hicho, kumpatia mradi mkubwa mwekezaji mwenye kiasi
hicho cha fedha, ambapo hata hapa nchini walikuwapo wawekezaji, ambao wangeweza
kuwekeza.
Alisema, ni dhahiri kulikuwa na ubabaishaji
huku akishangazwa na mwekezaji huyo, kulalamika hapati faida kwenye mradi huku
akidai kuwa amechukua mkopo benki kuuendesha. Alisema, mwekezaji huyo atakuwa
amewekeza kwa fedha zake na kusingizia kuchukua mkopo ili kututumia kama kigezo
cha kushindwa kupata faida kwa kuwa anarejesha fedha benki, lakini pia
alishangazwa kuchelewa kwa ujenzi wa bustani na hoteli kwenye eneo linalodaiwa
kuwa ni la mita za mraba 40,000 ilhali wameoneshwa eneo dogo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Kaboyoka alikasirishwa kwa kutotekelezwa kwa ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota
tatu tangu mwaka 2007, iliyotakiwa kuwa na ghorofa 10 na vyumba 1000, lakini
uongozi wa Mlimani City umesema utaijenga kwa kipindi cha mwaka mmoja tu. Kutokana
na mazingira hayo tata, kamati yake iliagiza waliosaini mkataba huo kwenda
mbele ya kamati yake bungeni. Pia, kamati hiyo iliagiza kufanyika kwa ukaguzi
wa hesabu ili kubainisha deni, ambalo chuo hicho kinadai mradi huo wa Mlimani
hadi sasa.
Awali akisoma ripoti ya mkataba huo,
Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji wa Chuo Kikuu hicho, Pancras
Bujulu alisema kuwa kwa miaka 10 ya kuanza kwa mradi, mwekezaji huyo amepata Sh
bilioni 16 huku chuo hicho kikidai Dola 340,000, fedha ambazo PAC imeona kuwa
ni ndogo na kuagiza ufuatiliaji zaidi ili kubaini deni halisi. Bujulu alisema
kuwa chuo hakijapewa haki stahili ya kufuatilia pato halisi, linalopatikana
kwenye mradi huo, kitu ambacho pia kiliwaudhi wabunge hao. Akitoa msimamo wa
chuo kwenye kamati hiyo, Profesa Anangisye alikiri kuwepo kwa upungufu mkubwa
kwenye mkataba huo na kuahidi kutoa ushirikiano stahiki kwa kamati hiyo.
No comments:
Post a Comment