Rais wa Tanzania, Dkt John Magufuli |
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya
Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais wa Tanzania ameagiza uchunguzi wa kina
ufanyike kwa meli zote 470 ambazo zimesajiliwa Tanzania na zinapeperusha
bendera ya Tanzania.
Agizo hilo limekuja
baada ya serikali ya Tanzania kufuta usajili wa meli mbili za kigeni wiki hii,
baada ya taarifa ya kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za
kulevya na silaha zikiwa zinapeperusha bendera ya Tanzania.
"Fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa
ambazo ni 5 na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinazoendelea kufanya kazi
zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwa na watu wanaofanya
mambo kwa maslahi yao." amenukuliwa Rais Magufuli.
Serikali ya Tanzania
imetangaza kuunda kamati ya pamoja ya wataalam bara na visiwani
itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitiwa upya
usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa
nchini, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na hatimaye kutoa mapendekezo na
ushauri kwa Serikali.
Aidha imebainika
kuwa wenye meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito
wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao.
No comments:
Post a Comment