I. UTANGULIZI:
Zao la kabichi hulimwa katika mikoa ya MorogKilimanjaro na Mbeya.
Kama mboga zao la kabichi lina viini lishe kama chokaa, protini, kambakamba na maji kwa wingi. Hutumika kutengeneza kachumbari, pia kuchanganywa na nyama au maharage.
II.HALI YA HEWA
Zao la kabichi hupendelea:-
- hali ya ubaridi
Mwinuko: Kuanzia mita 1200 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari.
Udongo: - - Tifutifu
- Rutuba nyingi na
- Unaohifadhi unyevu kwa muda mrefu
- Usiotuamisha maji
- Usio na chumvichumvi nyingi.
- Kama hauna rutuba ya kutosha ongeza mbolea ya samadi
au mbolea vunde.
III. AINA ZA KABICHI
· Early Jersey Wakefield:
- Umbo lilochongoka kidogo,
- Hufunga vizuri,
- Uzito ni kati ya kilo 1.5 hadi 2.0,
- Hukomaa mapema siku 90 – 100 tangu kupandikiza.
· Copenhagen Market:
- Vichwa vya mviringo na hupasuka kirahisi
- Hukomaa mapema, siku 90 – 100 tangu kupandikiza
· Prize Drumhead:
- Vichwa vikubwa (kilo 2- 2.5),
- Vichwa ni bapa, huchelewa kukomaa (siku 110 – 120)
- Huvumulia hali ya jua kali,
- Pia vichwa hupasuka.
· Oxheart:
- Vichwa vidogo huchongoka kama moyo,
- Hupendwa sana na walaji,
- Ladha yake ni tamu, hukomaa mapema,
- Hazina tabia ya kupasuka.
· Glory of Enkhuizen:
- Vichwa vya mviringo,
- Huvumilia hali ya jua kali,
- Huchelewa kukomaa (siku 110 – 120)
- Ina tabia ya kupasuka.
IV. KUOTESHA MBEGU:
Mbegu za kabichi huoteshwa kitaluni na baadaye huhamishiwa shambani. Andaa kitalu vizuri na weka mbolea za asili zilizooza vizuri kwa kiasi cha ndoo 5 – 10 za ujazo wa kilo 20 kwenye eneo la mita za mraba 10. Changanya na udongo kisha lainisha udongo kwa kuvunja mabonge makubwa kwa kutumia reki.
Tengeneza tuta lililoinuka kwa sentimita 25 na lenye upana wa mita 1. Mwagilia maji kwenye tuta siku moja kabla ya kusia mbegu. Kiasi cha mbegu zinazohitajika ni gramu 1 kwenye eneo la mita 1 ya mraba hivyo hekta 1 huhitaji gramu 200 – 300.
Sia katika umbali wa sentimita 15 toka mstari hadi mstari na kina cha nusu sentimita.Funika mbegu na udongo laini kasha tandaza nyasi kazu ili kuhifadhi unyevu.Mwagilia maji kila siku asubuhi na jioni mpaka mbegu ziote, huota kwa muda wa siku 5 – 10.
V.KUTAYARISHA SHAMBA
- Shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza.
- Katua ardhi kwa kina cha sentimita 30
- Lainisha udongo na tengeneza matuta
- Weka mbolea za asili kwa kiasi cha ndoo 2 kwa kila hatua moja au
- Mbolea iwekwe kwa kila shimo kwa kiasi cha kilo kwa shimo.
- Mbolea ya N.P.K. 5:15:5 yaweza kuwekwa kwa kiasi cha kijiko 1 cha
chai chenye gramu 5 kwa kila shimo.
VI.KUPANDIKIZA MICHE
Miche huwa tayari kupandikizwa shambani baada ya wiki 3 – 5 tangu kusia mbegu . Miche huwa na urefu wa sentimita 15 – 20.
Ng’oa miche kwa uangalifu na pandikiza kama ilivyokuwa kitaluni na hakikisha mizizi haipindi wakati wa kupandikiza.
Nafasi ya kupandikiza:
Hutegemea aina ya kabichi
– zenye vichwa vikubwa (Drumhead) ni sentimita 60 kutoka mche hadi mche na sentimita 75 toka mstari hadi mstari.
– Zenye vichwa vidogo (Oxheart) ni sentimita 40 – 50 kutoka mche hadi mche na sentimita 60 toka mstari hadi mstari.
– Umbali toka tuta moja na jingine ni sentimita 60.
– Muda mzuri wa kuotesha ni asubuhi au jioni
– Baada ya kupandikiza weka matandazo kama vile nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu kuota kwa urahisi.
VII. PALIZI
Zao la kabichi halina mizizi ya kina kirefu hivyo wakati wa palizi ni muhimu kuwa mwangalifu kwa kupalilia juu juu ili kuepuka kukata mizizi. Kuongeza matandazo husaidia kupunguza palizi a mara kwa mara..
VIII. UMWAGILIAJI
Kabichi hustawi vizuri zaidi iwapo kuna maji ya kutosha kwenye udongo. Mwagilia mara mbili au zaidi kwa wiki kutegemea hali ya hewa na aina ya udongo.
Kabichi ambazo hazikupata maji ya kutosha huchelewa kufunga na huwa na vichwa vidogo. Zikikosa maji kwa muda mrefu na zikapata maji mengi ghafla, vichwa hupasuka.
IX. MBOLEA
- Mbolea ya kukuzia (S/A) huwekwa baada ya 4 – 6 baada ya kupandikiza miche na kabla ya vichwa havijaanza kufunga.
- Kiasi cha kilo 80 huhitajika kwa eka moja.
- Kilo 40 ziwekwe baada ya wiki 4 – 6 na kilo 40 ziwekwe tena baada ya mwezi mmoja
- Mche mmoja huhitaji kiasi cha kidogo cha gramu 5
- Mbolea iwekwe kuzunguka shina umbali wa sentmita 10 – 15 kutoka kwenye shina.
Muhimu: Epuka kuweka mbolea nyingi, kwani husababisha vichwa visifunge vizuri (kabichi zinakuwa nyepesi)
x. KUBADILISHA MAZAO Kabichi nizao linalotumia virutubisho vingi kulinganisha na mboga nyingine,hivyo kabla ya kuotesha kabichi panda mazao jamii ya mikunde ili kuongeza rutuba. Baada ya kuvuna kabichi otesha mazao yanayotumia chakula kidogo kama vile karoti, radishi au lettuce. Kubadilisha mazao pia hupunguza kuenea kwa wadudu waharibifu na magonjwa.
XI. WADUDU WAHARIBIFU · Viwavi wa kabichi: Hawa ni viwavi wenye rangi ya kijani na alama ya mstari wa kung’aa mgongoni. Nondo hutaga mayai chini ya jani na baada ya kuanguliwa viwavi hawa hula sehemu ya chini ya jani na kucha ngozi nyembamba mfano wa dirisha la kioo. Ni muhimu kuwadhibiti viwavi hawa kwa sababu ndio wanaoleta madhara makubwa. Viwavi wa kabichi huzuiwa kwa kunyunyizia moja ya dawa zifuatazo:- Nogos, Permethrin,Dimethoate, Sevin W.P. na Sumicidin.
Nzi wa Kabichi: Mashambulizi hufanywa na kiluwiluwi mwenye rangi ya kijani au bluu. Hula majani yote ya kabichi na kubakisha vena au vishipa vya majani. Inzi wa kabichi wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa za Sevin, Dimethoate, Permethrin na Fenvalerate(sumicidin)
Sota: Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi wakati wa usiku. Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Carbaryl, Fenvalerate au Decis mara baada ya kuotesha. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu huyu kwa kumfukua na kumuua. Kisha pandikiza mche mwingine.
Vidukari au wadudu mafuta: - Wadudu hawa ni wadogo sana wenye rangi ya kijani, nyeusi au khaki. - Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. - Hufyonza utomvu wa mimea na husababisha majani kubadilika rangi na kuwa meupe au njano iliyopauka. - Mmea hudumaa na hatimaye hukauka. Zuia kwa kunyunyiza mojawapo ya dawa hizi Fenvalerate, Dimethoate, Karate, Nogos.
Minyoo Fundo: Ni minyoo wadogo wanaoishi ardhini na ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kusababisha kabichi kudhoofu na kushindwa kufunga vizuri. Mimea iliyoshambuliwa, mizizi yake huwa na nundunundu.
Kuzuia:- - Matumizi ya mbolea za asili kila msimu husaidia kupunguza kuzaliana kwa wadudu hao. - Tumia mzunguko wa mazao, usiotesha zao la jamii ya kabichi baada ya kuvuna kama vile kabichi ya kichina, koliflawa,n.k Otesha mboga kama vile karoti, radishi, vitunguu au mahindi. - Ondoa masalia yote shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu hawa na yachome moto.
XII. MAGONJWA: · Kuoza shingo:- - Husababishwa na vidudu vya bacteria ambavyo viko kwenye udongo. - Hushambulia kabichi na kuzifanya zibadilike rangi. - Kuoza na kutoa harufu mbaya. - Vidudu vidovidogo huonekana pia kwenye sehemu iliyooza.
Kuzuia:- - Epuka kujeruhi kabichi wakati wa kuvuna - Vuna kabichi wakati hakuna mvua - Usilundike kwa wingi na kwa muda mrefu. - Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha. - Ng’oa masalia, choma moto na lima shamba mara moja baada ya kuvuna - Tumia mzunguko wa mazao. ·
Uozo Mweusi:- - husababishwa na Bakteria - Majani hugeuka kuwa njano na baadaye kuwa kahawia - Majani huanza kunyauka kutoka kwenye kingo zake na kuacha alama ya “V” yenye rangi nyeusi isiyokolea. - Baadaye majani hunyauka na kupukutika - Kama ukikata jani au shina, mviringo mweusi huonekana kwenye vena.
Kuzuia:- - Badilisha mazao. Usipande kabichi au jamii yake kwa muda wa miaka 2 kwenye eneo lililoadhirika. - Otesha kabichi kwenye sehemu ambayo haituamishi maji. - Kitalu na mazingira yake viwe safi daima. - Punguza miche ili kupunguza msongamano. - Ondoa masalia yote baada ya kuvuna ya yachomwe moto. - Otesha mbegu zilizodhibitishwa na wataalam.
· Kuoza shina:- - Ni ugonjwa waukungu - Madoadoa yaliyodidimia yenye rangi ya kahawia huonekana kwenye shina karibu na usawa wa ardhi, ikifuatiwa na kuvimba kwa shina. - Baadaye uyoga mweusi huonekana kwenye uvimbe huo. - Uozo wa rangi ya kahawia huonekana ndani ya shina. - Majani huwa na madoa meusi ya mviringo yaliyozungukwa na uyoga mweusi.
Kuzuia:- - Otesha kabichi sehemu ambayo haituamishi maji - Badilisha mazao, usioteshe kabichi kwenye eneo lililoathirika kwa muda wa miaka 3. - Lima shamba mara baada ya kuvuna ili kuwezesha masalia kuoza haraka kabla ya kuotesha tena. - Ondoa kabichi zote zilizoshambuliwa shambani. - Tumia dawa ya kuzuia ukungu kama vile Ridomil.
· Uvimbe wa mizizi:- - Husababishwa na ukungu - Hushambulia mizizi na dalili zake ni kudumaa kwa mmea na majani kukunjamana - Baadae mmea huoza
Kuzuia:- Badilisha mazao shambani. ·
Madoa Meusi:- - Chanzo ni ukungu. - Majani huwa na madoa madogo madogo ya mviringo yenye rangi ya njano . - Baadae madoa huwa makubwa na hugeuka kuwa meusi.
Kuzuia:- - Badilisha mazao - Hakikisha shamba ni safi wakati wote - Ikibidi tumia dawa za ukungu kama vile Kocide,Cupro, n.k.
·
Ubwiri Vinyoya:- - Ni ugonjwa wa ukungu. - Hupendelea hali ya unyevunyevu na baridi kali. - Huanzia kwenye kitalu - Mabaka ya mviringo yenye rangi ya njano huonekana upande wa juu wa jani. - Baadae hubadilika na kuwa rangi ya zambarau iliyochanganyika na nyeupe upande wa chini wa majani.
Kuzuia:- - Tumia mzunguko wa mazao. - Hakikisha udongo hautuamishi maji na kitalu ni kisafi wakati wote. - Tumia za ukungu kama Zineb, Didhane, M45, Kocide, Topsin-M na Ridomil.
Kuoza shinaau Kinyaushi:- - Husababishwa na ukungu. - Hushambulia miche michanga - Miche iliyoshambuliwa huonyesha dalili za kukauka. - Miche mikubwa huonyesha dalili za kudumaa - Sehemu ya shina iliyo karibu na ardhi hulainika na kuwa rangi ya kahawia. Kuzuia:- -Punguza miche kama imesongamana. -Nyunyiza dawa ya ukungu Kama Didhane M-45, Ridomil, Topsin-M.
XIII. KUVUNA Kabichi hukomaa katika siku 60 mpaka 210 tangu kupandikiza miche. Hata hivyo muda wa kukomaa hutegemea ain aya kabichi.Uvunaji hufanyika kwa kukata shina sentimita 2 – 3 kutoka kwenye kichwa kwa kutumia kisu. Ondoa majani ya nje na acha majani 2 au 3 ya kijani kwa ajili ya kuzuia kabichi zisikwaruzike na kuoza wakati wa kusafirisha. Punguza urefu wa majani ili kurahisisha ufungaji. Ni muhimu uvunaji ufanyike asubuhi au jioni. Ondoa kabichi zilizooza au kuharibika wakati wa kuvuna, kisha panga zilizobaki kufuata daraja kama vile ndogo, za kati na kubwa.
Mavuno:- Kiasi cha tani 40 au zaidi za kabichi hupatikana kwa hekta moja kama zao limetunzwa vizuri.
XIV. HIFADHI Kabichi ni zao linaloharibika kwa haraka, hivyo halina budi kutumika mapema iwezekanavyo baada ya kuvuna. Kabichi kwa ajili ya kuuzwa zisafirishwe mara moja kwa walaji. Kama usafiri ni mgumu, zihifadhiwe kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha. Wakati wa kusafirisha, ziwekwe kwenye matenga au visanduku vya mbao vilivyo na matundu yanayoingiza hewa ya kutosha.
No comments:
Post a Comment