Dkt. John Magufuli- Rais wa Tanzania (Picha ya Mtandao) |
Rais
Dkt John Magufuli ameondoka leo jijini Dar es Salaam kwenda Kampala Uganda
kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).
Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo na viongozi
wengine walikuwepo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kumuaga Rais
Magufuli.
Katibu Mkuu
wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko amesema, mkutano huo wa siku mbili
unaotarajiwa kujadili masuala ya miundombinu ndani ya nchi sita za EAC, afya na
maendeleo kwa ujumla.
Nchi
wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa
taarifa ya Sekretarieti ya EAC kwa umma, mkutano huo unatarajiwa kushirikisha
wajumbe zaidi ya 1,000 wa ndani na nje ya nchi wanachama wa jumuiya.
Wakuu wa nchi
wanatarajiwa kujadili masuala ya miundombinu, fedha za tiba na maendeleo kwa
kutumia kaulimbiu ‘Kukuza na kapanua mtangamano kwenye miundombinu na maendeleo
ya sekta ya afya kwenye nchi wanachama EAC’.
Mkutano wa
Kampala umeandaliwa na sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na nchi wanachama
wa jumuiya hiyo, na wadau wakubwa wa maendeleo kwenye eneo hilo.
Utakuwa
mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi za EAC kuzungumzia masuala ya afya na
utakuwa wa nne kuhusu kugharamia miundombinu na maendeleo.
Mkuu wa
Mawasiliano kwenye Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno kupitia taarifa
yake amesema wakuu wa nchi wanatarajiwa kuzungumzia maendeleo ya miradi ikiwemo
miundombinu bora, ya uhakika, endelevu, imara na inayotolewa haraka ikiwemo wa
kieneo na ile ya kuvuka mipaka ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi na hali
bora za mwananchi.
No comments:
Post a Comment