Meno ya Kiboko (Picha ya Mtandao) |
Serikali imesema kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) itafanya mnada wa hadhara wa meno
ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.
Imesema mnada huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango
umepangwa kufanyika Januari 29, mwaka huu saa nne asubuhi katika Jengo la
Mpingo, Barabara ya Nyerere Jijini Dar es Salaam, zilipokuwa ofisi za Wizara ya
Maliasili na Utalii (Ivory Room).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Dk James Wakibara alisema katika taarifa yake kuwa mnada huo
utawahusisha wafanyabiashara wa nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la
Kwanza mwaka 2017.
Alisema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati
ya Januari, 25 na 26 mwaka huu kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu
jioni kabla ya siku ya mnada huo.
Amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa
asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia kulipwa ndani
ya siku 14 zijazo baada ya mnada huo.
“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa
kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka
kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,”
alionya.
Alisema meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo
bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa
kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu
na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.
No comments:
Post a Comment