Mnyama Pimbi |
Utangulizi,
Pimbi ni Mnyama au Mdudu?
Pimbi ni jamii ya wanyama wenye maumbile
madogo na vimo vifupi sana ambao wanapatikana maeneo mbalimbali hasa barani
Afrika.
Kwa hapa Tanzania utaweza kuowna katika
mikoa yenye Milima yenye Miamba na mapango , hasa mikoa ya Singida, Dodoma,
Iringa na kwingineko.
Ni
jamii moja tu ya pimbi ambayo inapatikana nje ya bara la Afrika na maeneo ya
ghuba za Arabuni kutokea nchi ya Lebanon hadi maeneo ya Saudi Arabia.
Wanyama hawa kutokana na maumbile yao
madogo huwa ni vigumu sana kuwaona na bila kuwa makini unaweza zunguka
hifadhini hata mwezi mzima bila kuwaona kwani huwa wana tabia ya kujificha sana
kwenye mazingira wanayoishi.
Hivyo unapokuwa unatalii katika hifadhi za
wanyamapori unapaswa kuwa makini zaidi katika uchunguzi hasa maeneo yenye
miamba.
Kabla hatujaingia kiundani zaidi katika kumjua Pimbi, napenda
ndugu msomaji utambue kuwa kuna jamii mbali mbali za Pimbi ambazo kwa utafiti
inasemekana kuna jamii tatu za wanyama hawa.
Jamii hizi ni kama ifuatavyo mbili kati ya
tatu hujulikana kama Pimbi wa kwenye miamba na moja ni Pimbi wa kwenye miti.
Jamii zote hizi hufanana sana kwa muonekano na ukubwa wa mwili.
Sasa leo napenda tutumie muda mfupi kuwajua PIMBI WA KWENYE
MIAMBA (ROCK HYRAX). Nakusihi kuwa pamoja na mimi mwanzo mpaka mwisho wa
uchambuzi wa pimbi hawa ili uweze kujifunza na kujua mengi kuhusu wanyama hawa
machachari sana.
SIFA NA TABIA ZA PIMBI WA KWENYE MIAMBA
Pimbi ni wanyama wanaofanana au kuonekana kama sungura kwani
wana miguu mifupi, mikia mifupi sana ( sawa na hawana mikia kabisa) na masikio
ya duara. Sifa hizi zimepelekea wanyama hawa kupewa jina la Sungura wa kwenye
miamba kwani wana fanana sana na sungura.
Dume na jike huwa wana fanana sana kwa ukubwa na huwa ni vigumu
sana kwa mbali kuweza kuwatofautisha kati ya jike na dume kutokana na kufanana
kwao. Hivyo kuweza kuwatofautisha kati ya jike na dume lazima uweze kuwashika
au kuwa karibu zaidi.
Pimbi ukiwachunguza vizuri katika nyayo za miguu na viganjani
wana alama kama vitufe vyenye matezi mengi sana ya jasho. Matezi na alama hizi
za vitufe huwasaidia wanyama hawa kuweza kukimbia na kushikilia kwenye miamba
vizuri wakati wana kimbia.
Kwa ujumla ukimchunguza vizuri utagudua ana alama nyeupe kwa juu
ya macho na sehemu ya juu anakuwa na rangi ya weupe wuepe inayoelekea kuwa kama
manjao. Rangi hii inaweza kuonekana kwa baadhi ya jamii nyingine za pimbi japo
huwa huwa haiwezekani kwa jamii moja kuzaliana na jamii nyingine.
Wana manyoa marefu yaliyo enea mwili mzima na yenye rangi ya
manjano au kijivu ifananyo na kahawia.
Pimbi pia wana matezi ya juu ambayo
yamezungukwa na rangi kama ya utadu wa maziwa au manjano na wakati mwingine
kahawia iliyokoza sana au mzunguko wa manyoa meusi ambayo husimama kipindi
pimbi anapokuwa na hasira.
Mbali na kuwa ni jamii ya wanyama wenye damu moto, lakini pimbi
ni wanyama ambao wana uwezo mdogo sana wa kurekebisha jotoridi la mwili na
kiasi kidogo sana cha mmeng’enyo wa chakula ukilinganisha za ukubwa wa miili
yao.
Jotoridi katika miili yao hurekebisha kwa njia
za kukusanyika pamoja, kukaa muda mrefu bila kufanya shughuli yoyote au wakati
mwingine kwa kujitutumua. Hivyo kitu cha kwanza kukifanya asubuhi wanapo amka
huwa wana lala kwenye miamba ili kupata joto.
Pimbi hawa huishi kwenye kundi ambalo huwa na kiongozi ambae ni
dume mtawala. Hii ni tofauti na pimbi wa kwenye miti ambao huishi kwa kujitenga
japo ni mara chache sana kuona kundi la pimbi wawili hadi watatu katika jamii
hii ya pimbi wa kwenye miti.
Pimbi wa kwenye miamba huwa wana uwezo wa kuona zaidi majira ya
asubuhi na mchana tofauti na pimbi wa kwenye miti ambao wao wana uwezo wa kuona
zaidi majira ya usiku.
Pimbi hutumia sehemu moja kwa kukojolea na haja kubwa. Pimbi
wote ndani ya kundi huwa na desturi ya kuchagua sehemu maalumu ya kukojoa na
haja kubwa na si kufanya hivyo kila mahali.
Huwasiliana kwa njia ya sauti za miguno, mngurumo au kama
filimbi na wakati huu kundi moja huweza kuliitikia kundi linguine popote
walipo.
UREFU, KIMO NA UZITO
Urefu= Pimbi hawa wa kwenye miamba huwa na urefu wa takribani
sentimeta sm 30 – sm 56
Kimo=hufikia kim cha sentimeta sm 23 – sm 30
Uzito= Pimbi hawa huwa na uzito wa hadi kilogramu kg 3 – kg 5
MAZINGIRA
Pimbi wa kwenye miamba wameenea sana barani Afrika. Hupendelea
kuishi kwenye miamba sana. Kwa hapa kwetu Afrika mashariki pimbi hawa
wanapatikana maeneo yenye muinuko wa futi takribani 14,000 kutoka usawa wa
bahari.
Ukitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha utaweza kuwaona wanyama
hawa vizuri sana kutokana na baadhi ya maeneo ya hifadhi hii kuwa na miamba
mingi sana.
CHAKULA
Pimbi hawa ni miongoni mwa jamii ya wanyama walao majani, hivyo
kwa ujumla tunasema chakula kikubwa cha wanyama hawa ni kile chenye asili ya
mimea Japo kuna wakati mwingine wanyama hawa hula wadudu na baadhi ya viumbe
jamii ya reptilian kama mijusi.
Huwa wanapenda kula majira ya asubuhi kabla jua halijawa kali
zaidi na desturi yao katika ulaji huwa wanakula kwa kutengeneza duara ili
kuweza kuona pande zote kwa ajili ya kuwaepuka maadui zao.
Na
maranyini pimbi hawa huwa wanakula maeneo ambayo yapo karibu sana na makazi yao
kwani inakuwa ni rahisi kukimbia na kujificha ndani ya miamba.
Vyakula ambavyo wanapendelea sana wanyama hawa ni majani,
matunda, wadudu, mijusi na wakati mwingine mayai ya ndege. Wana uwezo wa kuishi
muda mrefu sana bila kunywa maji kwani wanapata maji yakutosha sana kutoka
kwenye vyakula wanavyo kula.
KUZALIANA
Pimbi hawa huishi kwa makundi na makundi zaidi ya moja huweza
kuishi kwenye eneo moja. Pamoja na kundi zaidi ya moja kuishi kwenye eneo moja,
bado huwa kuna utawala kwa madume. Kila dume huwa na mipaka yake na anaweza
kumiliki hadi majike ishirini kwa wakati mmoja.
Jike huwa anazaa mara moja tu kwa mwaka na maranyingi wanyama
hawa hupandana majira ya joto kisha watoto kuzaliwa majira ya kipupwe. Mara
baada ya kupandana jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi saba hadi saba na
nusu. Hii inamfanya mnyama huyu kuwa ndo mnyama mwenye umbo dogo pekee ambae
anakaa na mimba kwa muda mrefu kulio wanyama wote wadogo duniani.
Katika familia moja majike wote wenye mimba wanapoanza kuzaa
basi watazaa na kumaliza wote ndani ya wiki tatu tu na kwa jamii hii ya pimbi
jike huzaa watoto kuanzia 1 – 4. Watoto huzaliwa wakiwa wamekamilika na huweza
kukimbia na kuruka mara tu baada ya saa moja tangu kuzaliwa.
Watoto huwa chini ya uangalizi kwa takribani
miezi mitano na wote kwa pamoja wakike na kiume huwa tayari kwa kuzaa wafikishapo
miezi 16 – 17.
Wafikishapo umri wa miezi 16 hadi 17 watoto wa kike hujiunga na
kundi la kina mama huku watoto wa kiume huanza kujiandaa kuondoka ndani ya
kundi hilo kutokana na kufukuzwa na madume na hapo ni kabla hawajafikisha miaka
mitatu ( yaani takribani miezi 30), japo wengi wao huondoka wakiwa na miezi 16
– 24. Maisha ya pimbi kutokana na tafiti mbali mbali huwa ni miaka 8 – 12.
UHIFADHI
Mpaka sasa pimbi wa miamba hawajawa kwenye mjadala wa kiuhifadhi
kutokana na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na uhifadhi wa
maumbile asili (International Union for Conservation of Nature- IUCN).
Hii
ni kutokana na kwamba wanyama hawa bado wametawanyika au kupatikana kwa wingi
katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori
. Japo jambo la kushtusha ni kwamba jamii
ya pimbi wa miti wamekuwa wakiwindwa sana hasa mkoani Kilimanjaro kutokana na
manyoa yao na nyama pia.
MAADUI NA CHANGAMOTO KWA PIMBI WA MIAMBA
Maadui wakuu wa wanyama hawa ni Simba, Chui, Fisi, Mbweha, ndege
kama Tai, na nyoka hasa Chatu wa kwenye miamba.
Mpaka sasa bado hakujawa na tishio kwa pimbi hawa. Nadhani ni
kwasababu wanapatikana sana maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori hivyo
wanakuwa na ulinzi wa kutosha.
Japo kwa jamii ya pimbi wa kwenye miti
tishio kubwa sana kwao ni uharibifu wa misitu kwani huathiri sana makazi yao.
HITIMISHO
Ni muhimu sana kuwajua wanyama hawa wadogo wadogo ambao
hawazungumziwi sana kwenye midomo ya watu kwani wanaonekana hawana mchango
wowote.
Nina
uhakika wengi mliosoma makala hii vizuri mlikuwahamjui kama pimbi ni mnyama
hasa kutokana na kuto tangazwa sana hapa nchini.
Wengi mlimfahamu pimbi kama katuni tu na
visa vyake kwenye magazeti “HARAKATI ZA PIMBI” sasa kupitia darasa hili umemjua
pimbi ni nani.
MUHIMU…Napenda nikudokezee kidogo umuhimu mkubwa sana wa wanyama
hawa, baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa mkojo na kinyesi cha pimbi ni dawa kubwa
sana ya ugonjwa wa KIFAFA.
Pili pimbi wana uwezo wa kula majani ambayo ni sumu
ka wanyama wengine hivyo husaidia kupunguza athari kwa wanyama ambao wangeweza
kula majani haya na kufa kitu ambacho ni hasara kubwa sana kwa taifa na uchumi
wetu kiujumla.
Hebu
fikiria wanakufa tembo au faru kwa kula majani ya sumu endapo tungekuwa hatuna
pimbi kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Kwa kuishirikisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi wa Wanyama
hawa inasaidia sana kutokomeza suala la ujangili ulio kithiri sana kwenye
hifadhi za wanyamapori.Mwisho wa makala hii ndo mwanzo wa makala ijayo endelea
kufuatilia makala kutia blog yako pendwa ya Nijuze News uendelee kujuzwa zaidi.
Kwa maoni
: Call,sms, whatsApp 0764228384,
No comments:
Post a Comment