Waarithiriwa wa Shambulio linalodaiwa kuwa la kemikali nchini Syria(GETTY IMAGE) |
Wachunguzi wa silaha za kemikali nchini Syria wataruhusiwa kuzuru katika eneo linalodaiwa kushambuliwa na silaha za sumu siku ya Jumatano, kulingana na Urusi.
Kundi hilo la kimataifa limekuwa nchini humo tangu siku ya Jumamosi lakini halijaruhusiwa kuingia Douma.
Shambulio hilo la siku ya Aprili 7 lilivutia shambulio dhidi ya serikali ya Syria lililotekelezwa kwa pamoja na Marekani, Uingereza na Ufaransa wiki moja baadaye.
Syria na mshirika wake Urusi wamekana shambulio lolote la kemikali huku Urusi ikitaja madai hayo kama 'yaliopangwa'.
Mapema siku ya Jumanne , chombo cha habari cha Syria kilisema kuwa ulinzi wa angani wa taifa hilo ulikabiliana na shambulio la makombora juu ya nga ya magharibi mwa mji wa Homs.
Makombora hayo yalilenga kambi za wanahewa wa Shayrat lakini haikusema ni nani aliyetekeleza mashambulio hayo.
Ripoti nyengine kutoka kwa wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran-Hezbollah ilisema kuwa mtambo wa ulinzi wa angani ulitungua makombora matatu yaliolenga kambi ya wanahewa ya Dumair, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Damascus.
Msemaji wa Pentangon aliambia Reuters : Hakuna shughuli za kijeshi za Marekani katika eneo hilo wakati huo.
Mapema siku ya Jumamosi saa za Syria, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilitekeleza mashambulio ya pamoja katika maeneo tofauti nchini Syria.
Operesheni hiyo ilikuwa ikijibu shambulio la silaha za kemikali iliotekelezwa na serikali ya Syria na kulenga raia na kuwaua makumi ya watu.
Wachunguzi kutoka shirika la kuzuia utumizi wa silaha za kemikali OPCW wako katika mji mkuu wa Damascus , lakini wamekuwa wakisubiri kuanza uchunguzi.
Wakati watakapowasili katika eneo hilo siku ya Jumanne, itakuwa siku 11 tangu shambulio hilo.
Wanatarajiwa kuchukua mchanga na sampuli kusaidia kutambua kemikalizilizotumika katika shambulio hilo.
Mjumbe wa Marekani katika shirika la OPCW hatahivyo ameonyesha wasiwasi wake kwamba Urusi ilitembelea eneo hilo na huenda iliharibu ushahidi ili kuzuia uchunguzi.
Lakini katika mahojiano na BBC, waziri wa maswala ya kigeni nchini humo Sergei Lavrov alisema: Nawahakikishia kuwa Urusi haijaharibu ushahidi wowote katika eneo hilo.
Alisema kuwa ushahidi uliodaiwa na Marekani , Uingereza na Ufaransa ulitokana na habari za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kwamba ushahidi kama huo ni kitu kilichapangwa.
Bwana Lavrov na wengine pia wamekosoa mataifa hayo matatu kwa kutekeleza mashambulio hayo kabla ya kundi la wachunguzi wa OPCW kufanya uchunguzi wao.
Wakati shambulio hilo lilipodaiwa kufanyika tarehe 7 Aprili, Douma, katika eneo la mashariki mwa Ghouta, lilikuwa eneo linalodhibitiwa na waasi karibu na mji mkuu wa Damascus baada ya mwezi mmoja wa mashambulio.
Kwa sasa mji huo uko chini ya udhibiti wa majeshi ya Syria na Urusi.
Mabomu mawili yaliokuwa na kemikali yalidaiwa kuangushwa saa kadhaa tofauti katika mji huo.
Duru za kimatibabu nchini Syria zinasema kuwa miili kadhaa ilipatikana ikitoa mapovu mdomoni mbali na kuwa na ngozi iliokosa rangi na macho yaliochomeka.
Duru za Marekani zinasema kuwa zilipima sampuli za mikojo na damu kutoka kwa waathiriwa na kufanikiwa kupata kemikali ya khlorine na gesi ya neva.
No comments:
Post a Comment