Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina |
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametibua na amekamata makontena matano yenye tani 100 za zao la mwani yenye thamani ya Sh bilioni 1.4 katika Bandari ya Dar es Salaam yakiwa tayari kwa ajili ya kutoroshwa kwenda Ufaransa huku mmiliki wa mzigo huo akiwa hana kibali wala leseni ya kusafirisha mazao hayo ya uvuvi kwenda nje ya nchi.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mpina alisema tayari serikali imeshaomba kibali cha
Mahakama ili kuwezesha tani hizo za mwani kuuzwa kwa njia ya mnada baada ya
mmiliki wake Kampuni ya Mari Culture kutojitokeza kwa zaidi ya wiki moja sasa
tangu mzigo huo ulipokamatwa.
Mpina alisema
Mari Culture imekiuka kifungu namba 65(1) cha Sheria ya Mazingira kwa kutaka
kutorosha mazao ya uvuvi bila kuwa na vibali vilivyoainishwa ambapo kwa
kuzingatia makosa hayo, imetozwa faini ya Sh milioni 100 kama Kipengele namba 191
cha Sheria ya Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004 kinavyoelekeza.
Aidha,
alisema serikali inahamasisha ukuaji wa shughuli za kilimo cha mwani na ndio
maana hata taasisi zake ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech)
zimekuwa zikifadhili mafunzo kwa wakulima ili kuchochea uchumi wao na Taifa kwa
ujumla, lakini haitavumilia wafanyabiashara wanaotumia njia za mkato
kusafirisha mazao hayo.
Hata hivyo
alisema kitendo cha kukwepa kutumia vibali vya serikali kimesababisha Taifa
kupoteza mapato mengi yatokanayo na zao hilo huku ikichangia kuikosesha
serikali takwimu sahihi zitokanazo na zao hilo linalotegemewa na wananchi wengi
wa ukanda mzima wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Pia Mpina
amewaonya wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi wanaondelea kufanya kazi hiyo bila
ya kuwa na leseni watambue kuwa watasakwa na kukamatwa kwani Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Rais John Magufuli iko makini katika kusimamia rasimali za
uvuvi zilinufaishe Taifa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwanaidi Mlolwa alisema
mmiliki wa mwani huo hakuwa na kibali cha kuchakata zao hilo wala leseni ya
kusafirisha nje ya nchi ambapo ni kinyume cha Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka
2003 na kanuni zake za mwaka 2009.
Alisema
Kanuni ya 13(1) kipengele (a-c) inaelekeza kuwa mtu yeyote haruhusiwi
kukusanya, kumiliki au kusafirisha mazao ya uvuvi kwa dhumuni la biashara bila
kuwa na leseni halali inayomruhusu kufanya biashara hiyo ambapo mtu yeyote
anayetaka kufanya biashara hiyo kwa kuzingatia vifungu hivyo.
Pia alisema
mtu yeyote haruhusiwi kusafirisha nje ya nchi mazao ya uvuvi bila kuwa leseni
hai iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi inayomruhusu kufanya biashara hiyo
ambapo pia mtu au kampuni inayofanya biashara ya mazao ya uvuvi inatakiwa
kuwasilisha marejesho kama kanuni namba 71(2) inavyoelekeza.
Mlolwa
alisema kutokana na kifungu namba 65(i) cha Sheria ya Mazingira Namba 20 ya
mwaka 2004 kinachotaka rasilimali zisimamiwe kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi ya
mwaka 2003 na kanuni zake na kwamba kampuni hiyo imekiuka kifungu namba 65(i)
cha Sheria ya Mazingira kwa kutaka kutorosha mazao ya uvuvi bila ya kuwa na
vibali vinavyotakiwa kisheria
No comments:
Post a Comment