.
Raia kadhaa wa Syria
wanatibiwa baada ya kushindwa kupumua kutokana na mashambulizi ya ndege
yaliyofanywa na serikali kwenye mji wa Saraqeb
Shirika linalofuatilia
haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza
limesema raia watano wanapatiwa matibabu kutokana na kukosa pumzi na kushindwa
kupumua baada ya serikali ya Syria kutumia silaha za sumu katika maeneo
yanayodhibitiwa na waasi kwenye mji wa Saraqeb uliopo kaskazini magharibi mwa
Syria.
Duru za kitabibu
zimeeleza kuwa wagonjwa wengine 11 walikuwa wakitibiwa kutokana na gesi yenye
sumu ya Chlorine, iliyotumika katika shambulizi hilo. Shambulizi hilo
limefanyika siku chache baada ya Marekani kuishutumu serikali ya Syria kwa
kutumia silaha za kemikali dhidi ya vikosi vya waasi karibu na mji mkuu,
Damascus.
Hata hivyo serikali ya
Syria imekanusha madai hayo ikiyaita kuwa ni ''uongo''. Siku ya Ijumaa Waziri
wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis aliwaambia waandishi habari kwamba serikali
yake ina wasiwasi gesi ya sarin huenda ikawa imetumika hivi karibuni nchini
Syria, ikizinukuu taarifa za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na
makundi ya waasi.
Marekani haina ushahidi
Hata hivyo, Mattis
alisema hana ushahidi kuhusu madai hayo. Mwezi uliopita watu 21 walitibiwa
kutokana na matatizo ya kupumua baada ya roketi kurushwa katika ngome ya waasi
Mashariki mwa Ghouta, nje kidogo ya Damascus.
Shirika hilo limesema
raia wengine 10 wameuawa katika jimbo la Idlib baada ya helikopta kushambulia
maeneo kadhaa, huku watu watano wakiwa na matatizo ya kupumua, kutokana na
taarifa kwamba gesi ya sumu ilitumika. Raia wengine wanne wameuawa na majeshi
ya serikali katika maeneo ya Maaret al Numan na Maasarin
.
Mji wa Saraqeb, Syria
Mkurugenzi wa vikosi
vya ulinzi wa raia, Abu Hamdo amesema ndege zinazoaminika kuwa za Urusi
zilishambulia hospitali ya Maaret al Numan na kusababisha uharibifu mkubwa.
''Ndege zimeanzisha
mashambulizi makali na kuharibu jengo la ghorofa saba na jingine la ghorofa
nne. Tumepata jumla ya miili sita na mtoto mmoja amejeruhiwa,'' alisema Hamdo.
Wakaazi wa Afrin
waandamana
Wakati huo huo,
mashirika ya misaada yamezionya nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria
kutowalazimisha kurejea nyumbani au kujadiliana hatua kama hizo. Ripoti
iliyotolewa na mashirika kadhaa ya kibinaadamu imeelezea kwamba maelfu ya
wakimbizi wako katika hatari ya kurejeshwa Syria mwaka huu, licha ya kuendelea
kwa ghasia na mashambulizi yanayohatarisha maisha ya raia.
Ama kwa upande
mwingine maelfu ya watu wameandamana jana katika mji wa Afrin, Syria wakiyataka
mataifa yenye nguvu duniani kuingilia kati na kusaidia kusimamisha mashambulizi
yanayofanywa na majeshi ya Uturuki dhidi ya Wakurdi na wameishutumu Urusi kwa
kuhusika na mauaji dhidi ya raia katika eneo hilo.
Januari 20, Uturuki na
waasi washirika wake walianzisha operesheni dhidi ya kundi la wanamgambo wa
Kikurdi nchini Syria, YPG, ambalo Uturuki imeliorodhesha kama kundi la kigaidi.
Uongozi wa eneo hilo umezitaka Marekani, Umoja wa Ulaya, Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa na majeshi yanayoongozwa na Marekani kuuzuia haraka uchokozi
wa Uturuki.
Hayo yanajiri wakati leo Rais wa Uturuki,
Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kukutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki
duniani, Papa Francis, ambapo pamoja na mambo mengine watajadiliana kuhusu
Syria na mzozo wa wakimbizi
No comments:
Post a Comment