![]() |
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi "Sigu" kushoto na kulia ni katibu wa chadema, Emmanuel Masonga, |
Mbeya.
Mabishano ya kisheria ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya umesababisha Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu kubakia mahabusu hadi Ijumaa.
mabishano hayo ya kisheria ulikuwa baina ya Mwanasheria wa Serikali na Wakili wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli. Wakili wa Serikali aliiomba mahakama hiyo isitoe dhamana kwa mshitakiwa kwa ajili ya usalama wake, huku wakili wa utetezi akipinga hoja hiyo na kuilazimu mahakama ya hakimu mkazi Mbeya kuamuru mbunge huyo kupelekwa mahabusu.
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite alitoa uamuzi huo jana katika kesi inayomkabili Mbunge Sugu na mwenzake, Katibu wa Chadema Kanda, Emmanuel Masonga ambapo alisema watuhumiwa hao watapelekwa mahabusu hadi Januari 19, mwaka huu mahakama hiyo itakapotoa uamuzi kama washitakiwa hao wanaweza kupewa dhamana ama la.
Hakimu Mteite alisema kuwa alikuwa na ziara ya kikazi ya kutembelea wilaya ambayo ataianza kesho, na Januri 19, mwaka huu atatoa uamuzi kama washitakiwa hao wanawezakupewa dhamana ama la. Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Joseph Pande kuwa watuhumiwa wote wawili wanashitakiwa kwa shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli kinyume cha sheria.
Akielezea tukio hilo lililotokea Desemba 30, mwaka jana katika viwanja vya shule ya msingi Mwenge Jijini Mbeya, Mwanasheria wa serikali Pande, alisema mtuhumiwa wa kwanza, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu akituhubia mkutano wa hadhara alidai kuwa kama Rais Magufuli anataka kupendwa asingemshuti Lissu au asingemfunga Lema miezi minne gerezani.
Pia asingemzuia yeye Sugu asiongee hili au lile, kwa kuteka watu. Alisema Sugu alinukuliwa akisema kuwa ‘Umemteka Roma, Ben Saanane mtoto wa watu hadi leo hatujui alipo’, alinukuu Wakili Pande na kuongeza kuwa siku hiyo hiyo katika eneo hilo hilo la Mwenge, mtuhumiwa wa pili, Emmanuel Masonga alidai katika mkutano huo kuwa hali ya maisha imekuwa ngumu, kila kona mambo yamekaza, watu wanatekwa mchana kweupe, watu wanauawa na kufungwa kwenye viroba mchana kweupe.
Alisema Masonga alidai kuwa Rais Magufuli ameamua kubadilisha namna ya kutawala, yeye anaamini njia ya kutawala Watanzania ni kuwaua, kuwazuia wasiongee, mbali na hayo alidai leo hii wanazuiwa, viongozi wa dini ndio wanaokwenda kuhakikisha nchi inakuwa na amani lakini utawala huu wa awamu ya tano unawazuia viongozi wa dini wasizungumze na kuwaonya.
Wakili Pande alidai Masonga aliueleza mkutano huo kuwa wana bahati mbaya kuwa na Rais ambaye hapendi kukoselewa, hapendi kuambiwa ukweli hivyo wanahitaji kuona namna ya kutoka wanakoelekea. Washitakiwa wote walikana kutenda kosa hilo ambapo Wakili Pande aliiomba mahakama hiyo isitoe dhamana kwa watuhumiwa hao kwa usalama wao kwa kuwa kuwa kosa walilofanya linahatarisha usalama maisha yao.
Alisema kuwa katika kipindi ambacho walikuwa nje kwa dhamana ya polisi, polisi walilazimika kufanya kazi ya kuwalinda na kwamba sehemu pekee wanayoweza kuwa salama ni mahabusu ambapo aliiomba mahakama izuie dhamana kwa watuhumiwa hao. Wakili wa utetezi, Sabina Yongo alipinga pingamizi la wakili wa Serikali kwa kile alichoieleza mahakama kuwa usalama wa watuhumiwa haupo shakani na kwamba kwa kuwa wao ni viongozi hawawezi kuruka dhamana na kosa wanaloshitakiwa nalo linadhaminika.
No comments:
Post a Comment