"Nabii" Tito |
DODOMA:
Mtu anayejiita Nabii Tito aitwa kwa mahojiano katika Kituo Kikuu cha Polisi
Mkoani humo.
Siku
za karibuni video zinazomuonesha mtu huyo akitangaza imani yake zimeenea sana
katika mitandao ya Kijamii
Viongozi wa
Dini wamejitokeza na kukemea vikali matendo ya Mtu huyo anayejiita 'Nabii Tito'
na kutaka Serikali iingilie kati suala
hilo baada ya Nabii huyo picha zake kuonekana amevaa vazi jeupe lenye alama za
msalaba kulia na kushoto.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria wa
Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba amesema hamtambui mtu anayejiita nabii
Tito na kwamba hajasajili kanisa lake katika ofisi ya msajili wa taasisi za
dini.
Komba amesema Serikali imeona vitendo anavyovifanya ‘nabii’
huyo kupitia mitandao ya kijamii na imeanza kuchukua hatua.
“Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu anayezuiwa kuongea
hapa nchini, mwache aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona anachokifanya na
yanayoendelea mitandaoni hatua zinachukuliwa dhidi yake,” amesema Komba.
Kauli hii imekuja kufuatia kusambaa kwa video mbalimbali
zikimuonyesha ‘nabii’ huyo akitoa
mafundisho yake huku akinywa vilevi pamoja na kufanya matendo ambayo ni kinyume
cha maadili ya dini, jambo ambalo limeonekana kuwakera wadau wengi wa dini.
Kwa upande wao viongozi mbalimbali wa dini wameonyeshwa
kukerwa na kulaani vitendo anavyovifanya mtu
huyo anayejiita ‘nabii’ na kusisitiza
kuwa hakuna dini inayoruhusu hayo.
Askofu Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema kuwa,
kutokana na vitendo anavyofanya, mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.
“Huyo
hawezi kuwa mtumishi wa Mungu na wala hafanyi huduma ya kanisa. Ni vyema watu
kama hawa wafuatiliwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Natumaini
Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani yake ina ofisi ya msajili wa taasisi za
dini itafanya kazi yake,” amesema
Mchungaji Lwiza.
Naye Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab
Katimba amesisitiza Serikali na viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo na
kueleza kuwa, hakuna kitabu chochote cha dini kinachohamasisha ulevi na ukosefu
wa maadili.
“Hilo
suala linakwenda tofauti na dini na mila na desturi zetu pia. Dini zinatakiwa
kuleta amani na kuhamasisha watu waheshimiane si kuzungumza mambo yanayokiuka
maadili yetu. Naona ipo haja ya viongozi wa dini na Serikali kuingilia suala
hili na waende mbali zaidi kwa kuongea naye huenda hafahamu anachokifanya,” amesema Rajab Katimba.
IGP Simon Sirro akimsikiliza mhubiri binafsi anayejiita
Nabii Tito ambaye jeshi la polisi la mkoani Dodoma limemtia mbaroni leo mjini
humo.
No comments:
Post a Comment